Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Raja Casablanca yameanza rasmi leo.
Robertinho amesema licha ya kuwakosa baadhi ya nyota ambao wapo kwenye majukumu ya timu za taifa lakini waliopo ni wengi na programu zinaendelea kama kawaida.
Robertinho amesema anafurahia uchezaji wa timu sababu wachezaji wanazidi kuelewa mbinu zake huku akitolea mfano mechi zetu tatu zilizopita tumefanya vizuri pia tumepata mabao mengi.
“Tumeanza maandalizi ya mchezo wetu ujao dhidi ya Raja, kuna wachezaji baadhi wapo kwenye majukumu ya timu za taifa lakini waliopo tunaendeleanao na programu za mazoezi.
“Jambo chanya ni kwamba tunacheza vizuri na tunapata mabao mengi. Wachezaji wameanza kuelewa mfumo mpya ambao tunautumia.”
Robertinho ameendelea kusema “sikuhizi tumebadili mfumo tunatumia washambuliaji wawili ambapo mabeki wapembeni Shomari Kapombe na Mohamed Hussein wanapanda juu kwenda kupiga krosi na mafanikio yameanza kuonekana katika mechi tatu zilizopita.”