Simba Queens imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Alliance Girls katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite Women’s Premier League SLWPL uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Queens ikifika langoni mara nyingi katika robo ya kwanza ya mechi.
Kinara Jentrix Shikangwa alitupatia bao la kwanza dakika ya 14 kwa shuti kali nje ya 18 lililomshinda mlinda mlango wa Alliance.
Dakika ya 28 Shikangwa tena alitupatia bao la pili kwa aina ile ile ya shuti kali nje ya 18 huku wachezaji wa Alliance wakiwa hawana la kufanya.
Asha Djafar alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga la tatu dakika ya 36 nae akipiga shuti kali nje ya 18.
Kocha Charles Lukula alifanya mabadiliko ya kuwatoa Wema Richard, Vivian Corazone, Zainabu Mohamed na Asha Djafar na kuwaingiza Olaiya Barakat, Joelle Bukuru, Asha Mwalala na Jackline Albert.
Queens imefikisha pointi 39 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 16 alama moja nyuma ya vinara JKT Queens.