Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya amesema maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Serengeti Lite Women’s Premier League (SLWPL) dhidi ya Yanga Princess utakaopigiwa Jumatano Uwanja wa Uhuru yanaendelea vizuri.
Makanya amesema kikosi kiliingia kambini moja kwa moja baada ya mchezo dhidi ya The Tigers Queens ambao tuliibuka na ushindi wa mabao 7-0.
Makanya ameongeza kuwa tumefanya maandalizi ya mchezo mapema kwakuwa tunajua utakuwa mgumu hasa ukizingatia mechi ya mzunguko wa kwanza ukimalizika kwa sare ya bao moja.
“Timu ipo kambini kwa takribani wiki sasa, baada ya mchezo wetu dhidi The Tigers Queens tulianza maandalizi ya mechi hii moja kwa moja kwakuwa tunajua umuhimu wa ushindi wake.”
“Mchezo utakuwa mgumu Derby siku zote haina mwenyewe na tofauti yetu ya pointi moja dhidi ya Fountain ndio inatufanya tuzidi kuwa makini na mchezo huu, lengo letu ni kuhakikisha tunachukua Ubingwa kwa mara ya nne mfululizo,” amesema Makanya.
Makanya amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa sapoti timu ili kutimiza malengo ya kuchukua ubingwa kwa mara ya nne mfululizo.
“Ni mechi kubwa na muhimu kwetu, tunahitaji sana kupata ushindi na hilo litakuwa gumu kama tusipopata sapoti ya mashabiki wetu, ndio maana tunawasisitiza waje kwa wingi Jumatano,” amesema Makanya.