Preview: Mchezo wetu dhidi ya Wydad

Leo saa nne usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Mohamed wa V nchini Morocco kuikabili Wydad Casablanca katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao moja tuliopata katika mechi ya mkondo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Aprili 21.

Wachezaji wapo kwenye hali nzuri wamepata maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wa leo wakiwa wanafahamu utakuwa mgumu kuliko ule wa mkondo wa kwanza.

Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema tutaingia kwenye mchezo wa leo kwa lengo moja la kucheza soka safi na kupata ushindi.

Katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tutaingia katika mchezo wa leo na mbinu tofauti ukilinganisha na mechi ya kwanza.

“Haiwezi kuwa sawa na vile tulivyocheza mechi ya kwanza ya nyumbani, lazima tutakuwa na mbinu tofauti sababu tupo ugenini.”

“Namuamini Mungu, pia nawaamini wachezaji wangu wataweza kufuata maelekezo tuliyowapa. Tumejipanga kucheza vizuri na kupata ushindi,” amesema Robertinho.

Kiungo mshambuliaji, Pape Sakho amesema wachezaji wako tayari kimwili na kiakili kupambana kuhakikisha tunatimiza malengo ya kufika nusu fainali.

“Sisi wachezaji tupo tayari, tumepata maandalizi ya kutosha, tupo tayari kukamilisha kazi tuliyoianza wiki iliyopita tukiwa nyumbani,” amesema Sakho.

Hali ya Kikosi..

Manula, Okrah, Ouattara, Sawadogo wabaki Dar

Wachezaji wetu Aishi Manula, Augustine Okrah, Mohamed Ouattara na Ismael Sawadogo hawatakuwa sehemu ya mchezo kutokana na kutokuwa timamu kimwili asilimia 100.

Nyota hao ambao afya zao zinazidi kuimarika wamebaki jijini Dar es Salaam kuendelea kufanya mazoezi binafsi wakisubiri kikosi kirejee wajiunge na wenzao.

Tumerudi tena Mohamed wa V…..

Aprili Mosi, 2023 tulishuka katika Uwanja wa Mohamed wa V kuikabili Raja Casablanca ambao ni wapinzani wakuu wa Wydad ambao tutacheza nao leo.

Katika mchezo huo tulipoteza kwa mabao 3-1 huku mshambuliaji Jean Baleke akifunga bao safi la kufutia machozi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER