Preview: Mchezo wetu dhidi ya Vipers

Leo saa moja usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kikosi chetu kitaikabili Vipers kwenye mchezo wa nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Tunarejea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tukiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Raja Casablanca katika mchezo uliopigwa Februari 18.

Viongozi, benchi la ufundi, wachezaji mpaka mashabiki tumeungana pamoja kuhakikisha tunapambana kurejesha heshima ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kurudisha hali ya ushindi.

Ushindi kwenye mchezo wa leo utarejesha matumaini yetu ya kufuzu…..

Endapo tutafanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo tutakuwa tumerejesha matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali kwakuwa tutakuwa tumefikisha pointi sita  huku tukiwa tumebakisha mechi mbili.

Ushindi wa bao moja tuliopata wiki iliyopita Entebe, Uganda umetuongezea nguvu na tupo tayari kupambana leo kujiweka nafasi nzuri zaidi.

Robertinho aridhishwa na maandalizi….

Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kikosi kimepata wiki moja ya maandalizi ya mchezo wa leo na wachezaji wapo kwenye hali nzuri.

“Tumepata muda mzuri wa maandalizi, wachezaji wapo tayari kwa mchezo. Timu inaendelea kuzoeana ingawa nina muda mfupi wa miezi mitatu tangu niwe hapa.

“Jambo chanya kwenye kutoka kwa wachezaji wangu nikuwa hali yao ya kujiamini iko juu, wanafanya vizuri mazoezini naamini leo tutafanya vizuri na kupata ushindi,” amesema Robertinho.

Kapombe atuma Ujumbe huu kwa Wanasimba…..

Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amekiri kuwa hatujafanya vizuri katika mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi lakini ni muda wa kurudisha heshima ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kupata ushindi dhidi ya Vipers.

“Tupo tayari kwa mchezo tumeandaliwa kimwili na kiakili kwa ajili ya mchezo wa leo, sisi wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunapambana kushinda na kurejesha heshima ya Uwanja wa Benjamin Mkapa,” amesema Kapombe.

Hali ya kikosi…..

Wachezaji wote wamefanya mazoezi ya mwisho jana asubuhi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na hakuna yoyote ambaye amepata majeraha yatakayomfanya kuikosa mechi ya leo.

Kocha Robertinho ameweka wazi katika Mkutano wa Waandishi wa Habari jana kuwa tayari anacho kikosi kamili ambacho kipo kamili asilimia 100 kwa ajili ya mchezo wa leo.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER