Preview: Mchezo wetu dhidi ya Polisi Tanzania

Leo saa 12 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex kuikabili Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Licha ya kwamba matokeo ya mchezo hayataathiri chochote kwetu katika msimamo tumejiandaa kuhakikisha tunashinda.

Katika mkutano wa Waandishi wa Habari kocha msaidizi, Juma Mgunda amesema mchezo wa leo tumeupa umuhimu mkubwa na lengo linabaki lile lile kubakisha alama tatu nyumbani.

Mgunda ameongeza kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kinachosubiriwa ni muda ufike tuingie uwanjani kupambania pointi tatu.

“Mchezo wa leo ni muhimu kama ilivyo mechi nyingine, ingawa matokeo hayatabili chochote kwetu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Mgunda.

Hali ya Kikosi….

Wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wamefanya mazoezi ya mwisho ya Gym kutokana na mvua kunyesha siku nzima ya jana hivyo isingewezekana kufanyika uwanjani.

Chama, Kanoute kuikosa Polisi….

Kiungo mshambuliaji Clatous Chama hatakuwa sehemu ya kikosi sababu amefungiwa mechi tatu kutokana na mchezo usio wa kiungwana aliofanya kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.

Kiungo mkabaji Sadio Kanoute pia hatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kwakuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye mchezo wa nusu fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Azam FC.

Tuliwafunga 3-1 Ushirika Moshi…..

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi uliopigwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Novemba 27, 2022 tuliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mabao yetu yalifungwa na nahodha John Bocco pamoja na Moses Phiri aliyefunga mawili.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER