Preview: Mchezo wetu dhidi ya Ihefu

Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Highland Estate kuikabili Ihefu FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunakutana na Ihefu zikiwa zimepita siku tatu tangu tuwafunge mabao 5-1 katika mchezo wa Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Matokeo ya mchezo uliopita tunategemea yataifanya mechi ya leo kuwa ngumu hasa ukizingatia Ihefu watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani.

Tunaingia katika mchezo wa leo huku kocha mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akitoka kuchukua tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu wa mwezi Machi na mshambuliaji Jean Baleke akichaguliwa mchezaji bora.

Mchezo wetu wa mwisho wa Ligi ulikuwa ugenini tulipocheza na Mtibwa Sugar, Machi 11 na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 ambayo yote yalifungwa na Baleke.

Hali ya Kikosi……

Kocha mkuu Robertinho ameweka wazi kuwa wachezaji wote ambao tumesafiri nao kwa ajili ya mchezo wa leo wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mapambano.

Wachezaji wote wamefanya mazoezi ya mwisho jana na wapo tayari kuhakikisha tunapambana kutafuta alama tatu.

Katika mchezo wa leo tutakosa huduma za nyota Henock Inonga, Shomari Kapombe na Aishi Manula ambao walipata maumivu kwenye michezo iliyopita wakati Augustine Okrah akiendelea kupata utimamu wa mwili.

Tuliwafunga Mzunguko wa kwanza….

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Novemba 12, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tuliibuka na ushindi wa bao moja.

Bao hilo pekee lilifungwa na kiungo mshambuliaji Pape Sakho.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER