Preview: Mchezo wetu dhidi ya Horoya

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Horoya kutoka Guinea katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Mchezo wa leo ni muhimu kwetu kupata ushindi ambao utatupa tiketi ya kufuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali bila kuangalia matokeo ya timu nyingine tulizonazo Kundi C.

Endapo tutashinda leo tutafikisha pointi tisa ambazo si Horoya wala Vipers ambao watazifikia hivyo sisi pamoja na vinara Raja Casablanca tutafuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi C.

Wakati kocha mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ akiongea na Waandishi wa Habari jana kuhusu mchezo huu amesema ingawa tunafahamu itakuwa mechi ngumu lakini tunapaswa kushinda.

Robertinho amesema anawaamini wachezaji wetu kutokana na ubora walionao na leo itakuwa kama fainali kwakuwa tunahitaji ushindi ili kujihakikishia kufuzu.

“Lengo letu ni moja kushinda na kuingia robo fainali, tunawaheshimu wapinzani wetu Horoya lakini tumejiandaa kikamilifu kuhakikisha tunashinda.

“Nawaamini wachezaji wangu, tumeweza kushinda mechi mbili nyumbani na ugenini dhidi ya Vipers na tumecheza vizuri pia hata kesho tutafanya hivyo siku zote mimi ni mtu chanya,” amesema Robertinho.

Walitufunga kwao….

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Jenerali Lansana Conte nchini Guinea, Februari 11 walitufunga bao moja.

Mchezo huko huo tuliongoza kwa umiliki wa mpira na tulipoteza nafasi kadhaa za wazi ambazo tungetumia hata moja tusingepoteza.

Ukiacha umuhimu wa pointi tatu ambazo tunazihitaji ili tufuzu robo fainali lakini tunahitaji kuwafunga Horoya ili kulipa kisasi pia.

Tutawakosa wawili….

Katika mchezo wa leo tutaendelea kuwakosa nyota wetu wawili Augustine Okrah na Mohamed Ouattara ambao ni majeruhi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER