Baada ya kupita takribani wiki tatu bila kucheza Ligi Kuu ya NBC leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Azam FC.
Mara ya mwisho kucheza ligi ilikuwa Februari 3, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipoifunga Singida Big Stars mabao 3-1.
Leo tunacheza Derby ya Mzizima, tunaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Azam na upinzani wanaotoa kila tunapokutana nao.
Hali ya kikosi…
Wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri morali ipo juu na wameshiriki mazoezi ya mwisho jana tayari kwa mtanange wa leo.
Hakuna mchezaji ambaye tutamkosa kutokana nakuwa majeruhi au kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Walitufunga mzunguko wa kwanza…
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Oktoba 27 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipoteza kwa bao moja lililofungwa na Prince Dube.
Robertinho awaamini wachezaji…
Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema anawaamini wachezaji wetu watapambana kuhakikisha tunashinda.
Robertinho amesema katika mchezo wa leo tunahitaji kupata ushindi utakao ambatana na kucheza soka safi la kuvuti.
“Tumewasisitiza wachezaji kuhakikisha tunatumia kila nafasi tutakayopata, tunahitaji ushindi na kucheza soka safi nawaamini wachezaji wangu,” amesema Robertinho.