Kocha Mkuu Pablo Franco, amesema hatukupata muda mzuri wa kujiandaa na mchezo wetu wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Uwanja wa Mkwakwani saa 10 jioni lakini tutahakikisha tunashinda.
Pablo amesema baada ya kumaliza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmerie timu imefanya mazoezi mepesi siku moja na leo itafanyika hivyo kabla ya kesho kushuka dimbani.
Pamoja na changamoto hiyo Pablo amesema kesho tutaingia uwanjani kwa lengo la kupambana ili kupata alama tatu muhimu ugenini.
“Ratiba inatubana sana, juzi tumetoka kucheza mechi ngumu ya kimataifa jana tumefanya mazoezi mepesi asubuhi mchana tukaanza safari ya huku. Tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi.
“Tutamkosa Nahodha John Bocco ambaye alipata maumivu kwenye mazoezi wakati tunajiandaa na mchezo dhidi ya Gendarmerie na Hassan Dilunga lakini wengine wote wako tayari kwa mchezo wa kesho,” amesema Pablo.
Kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto Gadiel Michael, amesema wao wapo tayari kuhakikisha wanapambana kupata alama tatu ingawa amekiri mchezo utakuwa mgumu.
“Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu, Coastal ni timu nzuri na ipo nyumbani kwa hiyo tutahakikisha tunapambana kupata alama tatu, kwa sasa kila mchezo ni fainali kwetu,” amesema Gadiel.