Mlinzi wa kati Joash Onyango ameweka wazi kuwa kitu pekee kilichopo vichwani mwa wachezaji kwa sasa ni kutetea taji la Ligi Kuu ya Vodacom na kushinda mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Onyango ambaye ni mmoja wa wachezaji waliokuwepo kwenye kikosi kilichocheza juzi dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika amesema dhamira yetu ni kuhakikisha tunatetea ubingwa wa ligi, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kushinda mechi ya robo fainali.
“Tunamshukuru Mungu tumemaliza salama hatua ya makundi ambapo tumemaliza tukiwa tunaongoza Kundi A, hivyo kwa sasa akili zetu tunawaza kutetea ubingwa wa ligi, FA pamoja na kushinda mchezo wa Robo Fainali wa Klabu Bingwa Afrika,” amesema Onyango.
Akizungumzia mchezo wa jana Onyango amesema wachezaji walipambana kutafuta ushindi na lakini jitihada zao hazikuzaa matunda na kujikuta tukipoteza ugenini.
“Tulivyoingia uwanjani tulikuwa na lengo la kutafuta alama tatu, ikishindikana tupate moja lakini mpira una matokeo matatu tunajipanga kwa michezo ijayo,” amesema Onyango.