Kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza amefunga mabao matano katika ushindi wa 6-1 tuliopata dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mshambuliaji Jean Baleke alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumizwa na kiungo wa Polisi, Salim Ally ‘Kipemba’ dakika ya 13.
Saido Ntibazonkiza alitupatia bao la kwanza dakika ya 15 kufauatia mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe kuokolewa na mlinda mlango kabla ya kumkuta mfungaji.
Dakika ya 20 Ntibazonkiza alitupatia bao la pili kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja nje ya 18 kufuatia Polisi kufanya madhambi eneo hilo.
Ntibazonkiza alikamilisha ‘hat trick’ dakika ya 26 kwa kutupia la tatu baada ya pasi safi kutoka kwa winga Peter Banda.
Mlinzi Israel Patrick alitupatia bao la nne dakika ya 66 akiwa ndani ya sita baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Kapombe.
Ntibazonkiza alitupatia bao la tano dakika ya 78 baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Polisi kufuatia pasi safi iliyopigwa na nahodha John Bocco.
Enock Mayala aliwapatia Polisi bao la kufuatia machozi dakika ya 85 baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Idd Kipagwile.
Ntibazonkiza alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga la sita dakika ya 89 baada ya mpira wa krosi uliopigwa na Kapombe kumgonga Kibu Denis kabla ya kumkuta mfungaji.
Ntibazonkiza amefikisha mabao 15 ya ligi akizidiwa moja na kinara Fiston Mayele huku mchezo mmoja ukiwa umebakia.
X1: Ally, Kapombe, Israel, Kennedy, Inonga, Erasto, Banda (Jimmyson 79′), Mkude, Baleke (Bocco 16′) Ntibazonkiza, Kibu.