Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amesema mashindano ya Super Cup huenda yakafanyika mwanzoni mwa mwaka 2022.
Akizungumza katika Twitter Spaces jana usiku, Barbara alisema lengo la mashindano hayo litakuwa ni kuiandaa Simba kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Barbara alikuwa akijibu maswali kutoka kwa watumiaji wa mtandao wa twitter waliotaka kujua kama mashindano hayo yatafanyika mwaka huu.
Barbara alisema wakati wanaanzisha Super Cup - iliyofanyika kwa mara ya kwanza msimu uliopita, lengo halikuwa kuifanya sambamba na tukio la Simba Day.
"Wazo la Super Cup halikuwa kwa ajili ya kwenda sambamba na Simba Day. Lengo lilikuwa kuiandaa timu pale inapokuwa inajiandaa kucheza hatua ya makundi. Lengo hilo liko palepale endapo tutaingia tena kwenye hatua ya makundi msimu huu," alisema.
Jana usiku, Simba iliandaa majadiliano maalumu katika twitter spaces yaliyokuwa na lengo la kuzungumza kuhusu Simba Day, Simba App na uzinduzi wa jezi.