Kocha Mkuu wa timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens, Hababuu Ally amesema hatutaidharau Timu ya FAD FC kutoka Djibouti katika mchezo wa mwisho wa kundi A ambao utatoa hatima yetu ya kutinga nusu fainali.
Hababuu amesema FAD ni timu pekee ambayo wachezaji wanahamasishana na wanajitahidi kupata matokeo hivyo haiwezi kuwa mechi rahisi na tumejipanga kuwakabili.
Kocha huyo ameongeza kuwa pamoja na ubora wa wapinzani hao lakini tumejipanga kuhakikisha tupata ushindi ambao utatupa tiketi ya kutinga nusu fainali.
"Mechi ijayo dhidi ya FAD itakuwa ngumu, nimeiona FAD kwanza timu yao ndiyo pekee kila mchezaji anaongea uwanjani kuhamasisha ingawa walipoteza mechi ya kwanza lakini hatuwezi kuidharau tutaingia uwanjani kutafuta alama tatu ili kutinga nusu fainali," amesema Hababuu.
Mchezo huo muhimu kwetu utapigwa Ijumaa, Septemba 3 katika Uwanja wa Moi Kasarani saa saba mchana.