Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola, amesema kikosi kipo kamili tayari kwa mchezo wetu wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KMC utakaopigwa saa moja usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Matola amesema tumejiandaa vizuri ingawa tunaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa KMC lakini tutaingia tukiwa na lengo kutafuta alama tatu.
Matola ameongeza kuwa katika mchezo wa kesho tutakosa huduma ya mlinzi wa kati, Joash Onyango ambaye amechelewa kujiunga na wenzake mazoezini.
“Mchezo utakuwa mgumu, tunaiheshimu KMC ni timu nzuri lakini inatupa changamoto kubwa kila tunapokutana nao lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata alama zote tatu,” amesema Matola.
Kwa upande wake Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema morali yao ipo juu na wanafahamu umuhimu ushindi katika mchezo huo huku akiwaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mchezo kila mmoja ambaye atapangwa kuanza atakuwa tayari kupambana kuipigania Simba, morali yetu ipo juu, tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kushinda,” amesema Zimbwe Jr.