Matola: Tupo tayari kwa Derby Kesho

Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya watani Yanga utakaopigwa kesho saa 11 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Matola amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri na morali zipo juu na tutaingia kwenye mchezo huo kwa lengo la kupambana na kupata pointi tatu.

Matola ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani kwa sasa lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunawakabili.

Akizungumzia kuhusu ubingwa Matola amesema bado tupo kwenye mbio za kupigania na hatuwezi kukata tamaa mpaka mwisho.

“Kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, hii ni Derby na mara zote haijawahi kuwa rahisi. Yanga ni timu bora na kila mtu anajua lakini tupo tayari kuwakabili.

“Tunafahamu mara ya mwisho tulipokutana hatukuwa bora lakini mechi ya kesho ni mpya, na kuna dakika 90 nyingine kabisa na hatutafanya makosa ambayo yataweza kutugharimu,” amesema Matola.

Kwa upande wake mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema wao kama wachezaji wapo tayari kupambana ili kuwapa furaha mashabiki.

“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tutahakikisha tupambana kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER