Licha ya wapinzani wetu katika hatua 64 bora ya CRDB Federation Cup Kilimanjaro Wonders kuwa timu ya daraja la chini lakini hatutaidharau badala yake kesho tutacheza kama fainali.
Kauli hiyo imetolewa na Kocha Msaidizi, Seleman Matola mbele ya Waandishi wa Habari wakati akizungumzia mchezo huo ambao utapigwa kesho saa 10 jioni katika Uwanja wa KMC Complex.
Matola amesema tunauzoefu wa kucheza na timu za madaraja ya chini ambazo kwa nyakati tofauti zilitufanya kukosa furaha kwahiyo tumejifunza na kila mchezo kwetu ni fainali.
“Wapinzani wetu hawana jina kubwa kama sisi lakini hatuwadharau na tutacheza kama tunavyocheza na timu nyingine yoyote ili kupata ushindi,” amesema Matola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin amesema malengo ya timu msimu huu ni kuchukua kila taji kwahiyo kila mchezo lazima tushinde.
“Tunahitaji kushinda kila mchezo ili kufanikiwa kutimiza malengo yetu ya kuchukua taji hili msimu huu, itakuwa mechi ngumu na Kilimanjaro Wonders hatuwajui lakini tumejipanga kuwakabili,” amesema Mzamiru.