Baada ya kukamilisha mechi mbili za kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika leo saa 2:30 usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar kuikabili Azam FC.
Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa tunafahamu tunaenda kukutana na upinzani mkubwa kutokana na ubora walionao Azam.
Iko wazi kuwa haitakuwa mechi rahisi lakini tutaingia uwanjani kwa lengo la kupigania alama tatu.
Kocha Fadlu atoa neno…..
Fadlu amesema ameitazama Azam katika mechi tatu zilizopita chini ya kocha wao mpya na kubaini kuwa wamebadilika kiuchezaji lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri na kuibuka na pointi zote tatu.
“Wachezaji wangu wameonyesha jambo chanya katika mchezo uliopita ambapo tulitoka nyuma kwa bao moja na kusawazisha na kuongeza mawili hilo linaongeza morali kwa timu kuelekea mchezo wa kesho,” amesema Kocha Fadlu.
Awesu aongea kwa niaba ya wachezaji…..
Kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu amesema kila mmoja atakayepata nafasi yupo tayari kuipambania timu na lengo likiwa kuchukua pointi zote tatu.
Awesu ameongeza kuwa amefurahi mechi hiyo kupelekwa katika Zanzibar kwakuwa atakuwa anacheza katika ardhi ya nyumbani na endapo mwalimu atampa nafasi ya kucheza amejipanga kuonyesha uwezo mkubwa.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo, tunaamini utakuwa mgumu lakini tumejipanga na matumaini yetu mashabiki watakuja kwa wingi kutupa sapoti,” amesema Awesu.
Tutawakosa Kagoma na Mzamiru……..
Katika mchezo wa leo tutawakosa viungo wakabaji Yusuph Kagoma na Mzamiru Yassin ambao ni majeruhi.
Ni mara ya kwanza mechi ya Ligi kupigwa New Amaan Complex……
Katika historia ya Ligi Kuu ya NBC hii itakuwa mechi ya kwanza kupigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar nasi tumeingia kwenye historia hiyo.
Mara ya mwisho tuliwafunga Azam uwanja wa New Amaan Complex………
Tulipokutana kwa mara ya mwisho katika Uwanja wa New Amaan Complex tuliibuka na ushindi wa bao moja katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano uliopigwa Aprili 27.
Bao hilo pekee lilifungwa na kiungo mkabaji Babacar Sarr aliyefunga kwa kichwa dakika ya 76 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.