Leo saa 12 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa CCM Mkwakwani kuikabili Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mechi iliyopita.
Tunafahamu ligi imeingia duru ya pili na kila timu inahitaji kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri nasi tumeliona hilo na tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo chanya kila mchezo.
Hiki ndicho alichosema Matola kuelekea mchezo wa leo…..
Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema wachezaji wote tuliosafiri nao wapo kamili na tutaingia kwenye mchezo kwa lengo la kutafuta pointi tatu ugenini.
Aidha Matola ameongeza kuwa utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora walionao Coastal hasa ukizingatia wapo nyumbani lakini tumejiandaa vizuri kuwakabili.
“Itakuwa mechi ngumu, Coastal ni timu bora kwa sasa. Kuna mapungufu yalionekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons tumeyaona na tumeyafanyia kazi.” amesema Matola.
Benchikha kuikosa Coastal Leo…..
Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha hataliongoza benchi la ufundi kwenye mchezo wa leo kutokana na kwenda nchini Algeria kwenye kozi ya ukocha.
Benchikha ameondoka nchini Machi 7 kuelekea Algeria kwa ajili ya kozi hiyo ambayo inachukua siku tano kabla ya kumalizika.
Wachezaji wapo tayari kwa mchezo………
Mlinda mlango, Ally Salim amesema kwa upande wa wachezaji wapo tayari kupambana kuhakikisha tunashinda.
Ally amesema tunajua mashabiki wetu wameumia kutokana na matokeo tuliyopata kwenye mchezo uliopita kwahiyo tumejipanga kuwapa furaha.
Tuliwafunga Coastal tulivyokutana mara ya mwisho…….
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru Septemba 21 mwaka jana tuliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0.
Mabao yote matatu kwenye mchezo huo yalifungwa na mshambuliaji Jean Baleke.