Leo tunamaliza kazi tuliyoianza Ndola

Baada ya kupita majuma mawili leo tunakamilisha kazi tuliyoianza Ndola, Zambia kwa kuikaribisha Power Dynamos katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Azam Complex saa 10 jioni.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Levy Mwanawasa, Septemba 16 ulimalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2.

Hatuna jambo jingine lolote leo zaidi ya kukamilisha kazi tuliyoianza na kuhakikisha tunashinda ili kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunakubali Power Dynamos walitupa upinzani mkubwa na walikuwa bora katika mchezo uliopita hasa kipindi cha kwanza lakini leo tumejipanga kuwakabili.

Robertinho aanika kila kitu….

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema wazi leo tunaingia uwanjani kwa lengo moja tu la kuhakikisha tunashinda na kuingia hatua ya makundi.

Robertinho amesema anakiamini kikosi chake na anatarajia ushindi ambao utatupa tiketi ya kuingia makundi ingawa amekiri haitakuwa kazi rahisi.

“Tumepata muda mrefu wa kujiandaa na mchezo wa leo, wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana kutafuta ushindi utakaotupeleka hatua ya makundi na hilo ndio lengo kuu,” amesema Robertinho.

Chama asema tupo kamili…..

Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama amesema kila mchezaji yupo tayari kupambana kwa ajili ya kuipigania timu kupata ushindi kwenye mchezo wa leo.

Chama ameongeza kuwa wanafahamu matumaini na furaha ya Wanasimba wanayo wao hivyo watahakikish hawawaangushi kwa namna yoyote.

“Sisi wachezaji tunajua umuhimu wa mchezo wa leo, tunafahamu furaha ya mashabiki wetu inatutegemea kwahiyo tutajitoa kuhakikisha hilo linatokea ingawa tunajua tutapata upinzani mkubwa,” amesema Chama.

Manula, Inonga, Kramo kuikosa Dynamos…..

Nyota wetu watatu, Aishi Manula, Henock Inonga na Aubin Kramo ndiyo wachezaji pekee ambao tutawakosa kwenye mchezo wa leo kutokana nakuwa majeruhi.

Manula tayari amerejea kikosini lakini bado anafanya mazoezi peke yake huku afya yake ikizidi kutengemaa na yupo mbioni kurudi langoni.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER