Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally ameiongoza Idara yake kutoa zawadi ya jezi kwa kuipongeza Azam TV kufikisha miaka 10 ya kurusha matangazo ya runinga.
Akikabidhi zawadi hiyo kwa uongozi wa Azam, Ahmed amesema Azam TV imeleta mageuzi makubwa katika soka la Tanzania kwa kuifanya Ligi Kuu ya NBC kuwa bora na kuwafanya wachezaji kuonekana zaidi kunakowapatia madili mbalimbali.
Amesema Azam TV inafanya kazi zao kwa ubora na ufanisi mkubwa na kila siku wamekuwa wakikua na wanaenda sanjari na mfumo wa kidigitali.
“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti, Wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba naipongeza Azam TV kwa kutumiza miaka 10 ya kutoa huduma kwa ubora mkubwa na pasi na shaka mmeleta mageuzi makubwa katika ligi yetu.
“Udhamini wa haki ya matangazo ni mkubwa ushindani umeongezeka kwenye ligi, mmekuwa msaada mkubwa kwa timu katika gharama za uendeshaji hilo pia ni jambo kubwa kwa Azam TV mmelifanya,” amesema Ahmed.
Kwa upande Msimamizi Mkuu wa Idara ya Michezo ya Azam TV, Christina Korroso ameushukuru uongozi wa klabu kwa kuthamini mchango wao huku akituomba kuendelea na utaratibu huu wa kuwatambua wanaofanya vizuri.
“Kipekee tunaushukuru Uongozi wa Simba kwa kuonyesha thamani kwetu, tumetimiza miaka 10 ya urushaji wa matangazo ya runinga na weledi mkubwa na tunaahidi kuendelea hivi,” amesema Christina.