Kauli ya Nahodha Simba Queens kuelekea mchezo wa kesho

Nahodha wa timu yetu ya Wanawake Simba Queens, Violeth Nicholaus amesema mchezo wa kesho dhidi ya FAD FC utakuwa mgumu kutokana na uhitaji wa alama tatu kutoka kwa kila timu.

Mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Moi Kasarani hapa nchini Kenya saa saba mchana sawa na ule wa Lady Doves dhidi ya PVP FC ambao utapigwa Uwanja wa Nyayo na kukamilisha hatua ya makundi.

Violeth amesema michuano ni migumu na kila timu imejipanga huku viwango vya wachezaji vikiwa havijapishana sana kitu ambacho makocha wamekiona na wanakifanyia kazi mazoezini.

Nahodha huyo ameongeza kuwa kila timu inayokutana nasi inajipanga vilivyo kutukabili kutokana na mafanikio tuliyopata ya kuchukua ubingwa wa Tanzania mara mbili mfululizo.

“Sisi kama wachezaji tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho na kuingia nusu fainali, kiukweli mashindano ni magumu na kila timu imejipanga ila lengo letu ni moja kushinda ubingwa,” amesema Violeth.

Simba Queens inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na alama nne sawa na vinara Lady Doves ya Uganda lakini ikitofautiana uwiano wa mabao.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER