Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema kuelekea mchezo wa kesho wa robo fainali ya CRDB Federation Cup dhidi ya Mbeya City tutapanga kikosi kamili na hakuna mchezaji atakayepumzishwa.
Matola amesema mchezo wa kesho utakuwa ni kama fainali kwakuwa tunahitaji kushinda ili kufuzu hatua ya nusu fainali na haitakuwa mechi rahisi.
Matola ameongeza kuwa Mbeya City ni timu imara na ipo kwenye kiwango bora kwa sasa lakini tumechukua tahadhari zote kwa ajili ya kuwakabili ili kuweza kutinga nusu fainali.
“Tunafahamu Mbeya City ni timu nzuri na ipo kwenye kiwango bora, wametoka kuwatoa Azam FC na kufika hatua hii kwahiyo sio timu ya kubeza hivyo tumejiandaa vizuri kuwakabili.”
“Kuhusu hali ya kikosi, wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na hatufikirii kupumzisha mchezaji yoyote kwakuwa tunaitaka nusu fainali,” amesema Matola.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ amesema tutaingia kwenye mchezo wa kesho tukiwa tunafahamu tunaenda kukutana na timu ngumu lakini tupo tayari kupambana ili kupata ushindi.
“Kila mchezaji atakyepata nafasi ya kucheza mechi ya kesho atakuwa tayari kuwajibika na kufuata maelekezo ya walimu ili kuisaidia timu kutinga nusu fainali. Tunaiheshimu City ni timu bora lakini tumejiandaa kuwakabili,” amesema Duchu.
Mchezo huo ambao utapigwa katika Uwanja wa KMC Complex umepangwa kuanza saa 10 jioni.