Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba yamekamilika.
Fadlu amesema baada ya kikosi kufika Kagera jana kilifanya mazoezi ya utimamu wa mwili na leo kitafanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Kaitaba na kesho tutashuka dimbani.
Akizungumzia mchezo wenyewe kocha Fadlu amesema utakuwa mgumu huku akiweka wazi kuwa tumekuwa tukipata wakati mgumu katika Uwanja wa Kaitaba lakini kesho itakuwa ni vita ya wachezaji 22 na atakayekuwa bora ataondoka na pointi tatu.
Kocha Fadlu amesema historia ipo kwenye mpira lakini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kushinda licha ya ligi kuwa ngumu.
“Tupo tayari kwa mchezo wa kesho, tunajua Kagera ni timu nzuri na inacheza soka la kisasa na mashambulizi yao yanajengwa kuanzia nyuma lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Kocha Fadlu.
Kwa upande wake mlinda mlango, Ally Salim amesema pamoja na ukweli kwamba Uwanja wa Kaitaba umekuwa mgumu kwetu kupata pointi tatu lakini wachezaji hawana presha juu ya hilo.
“Tumewahi kukutana na Viwanja vigumu kama ilivyo Kaitaba na bado tuliweza kupata ushindi hata kesho tunaweza kufanya hivyo, kikubwa tunahitaji mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kutupa sapoti,” amesema Ally.