Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo wa kesho dhidi ya APR wa kilele cha Simba Day utakuwa mzuri ambao utatupa picha kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Kocha Fadlu amesema itakuwa jambo zuri kupata ushindi kwenye mchezo wa kesho kutokana na kuwa na sherehe lakini atawapa nafasi wachezaji wote ili kuzoea mazingira ya kucheza katika wingi wa mashabiki.
Kocha Fadlu ameupongeza Uongozi wa klabu kwa kusajili wachezaji bora wenye umri mdogo ambao wana nguvu na ari ya kuipambania Simba kufikia malengo tuliyojiwekea.
“Kikosi kipo kwenye hali nzuri, mchezo wa kesho utakuwa kipimo bora kwetu, tunafahamu mashabiki watajitokeza kwa wingi uwanjani nasi tunaona itakuwa jambo zuri kuwapa furaha ya ushindi.”
“Ninafahamu Simba haijatwaa taji la ligi kwa miaka mitatu lakini safari hii tuna timu bora ambayo najivunia kuwa itatupeleka kwenye malengo tuliyojiwekea,” amesema Kocha Fadlu.
Kwa upande wake nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewatoa hofu Wanasimba na kuwaambia kuwa tuna timu imara ya ushindani na kesho wataanza kupata furaha waliyokuwa wanaisubiri.
“Tupo tayari kwa mchezo wa kesho, tunajua kuwa ni sikukuu ya Wanasimba na tiketi zimeisha siku tatu kabla kwahiyo wachezaji tunajua tuna jambo kubwa la kufanya,” amesema Zimbwe Jr.