Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha amesema kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa tatu usiku.
Benchikha amesema kila mmoja anajua ukubwa na ubora wa Al Ahly lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda katika mchezo wa nyumbani ili tuwe kwenye mazingira mazuri katika mchezo wa marudiano.
Benchikha amesema itakuwa mechi ngumu na tutaingia kwa tahadhari zote lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele hatua ya nusu fainali.
“Timu iko tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tumepata muda wa kujiandaa kwa ajili ya kuwakabili Al Ahly.
“Tunajua itakuwa mechi ngumu kwakuwa tunakutana na timu bora na yenye rekodi nzuri Afrika lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Benchikha.
Akizungumzia kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho na kila mmoja amejipanga kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo chanya.
“Kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari kuipambania Simba kupata ushindi, tunajua haitakuwa mechi rahisi lakini tumejipanga na lengo ni kutinga nusu fainali,” amesema Kapombe.