Mlinzi wa kulia Shomari Kapombe, ameweka wazi kuwa malengo yetu ya kufika hatua za juu katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika sasa tumehamishia Kombe la Shirikisho.
Kapombe amesema tulikuwa na mipango ya kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa lakini baada ya kushindikana sasa tumehamishia nguvu zote katika mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Akizungumzia mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi dhidi ya Asec Mimosas utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili wiki hii, Kapombe amesema utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda nyumbani.
Kapombe ameongeza kuwa wachezaji wote wako katika hali nzuri maandalizi yanaendelea vizuri na kwa muda uliobaki kuelekea mechi utatosha kutuweka fiti kabla ya kushuka dimbani Jumapili.
“Mwanzoni tulitaka kufika nafasi za juu katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini baada ya kushindikana tumehamishia nguvu katika Kombe la Shirikisho. Tunataka malengo tuliyokuwa nayo tuyakamilishe.
“Wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunawapa furaha mashabiki wetu kwa kufanya vizuri katika michuano hii. Tunawaheshimu Asec ni timu bora tunaifuatilia inaongoza ligi ya kwao lakini tumejipanga vilivyo kuwakabili na hatimaye tubakishe pointi tatu nyumbani,” amesema Kapombe.
One Response