Kikosi chetu kimefanikiwa kuondoka na alama zote tatu mbele ya Kagera Sugar baada ya kuifunga mabao 2-0 mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tulianza mchezo kwa kasi ambapo dakika 10 za mwanzo tulikuwa tumefika zaidi ya mara nne katika lango la Kagera.
Dakika ya 13 Kibu Denis alitupatia bao la kwanza baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Rally Bwalya.
Nahodha John Bocco alitupatia bao la pili dakika ya 29 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bwalya kufuatia shambulizi lililoanzia nyuma.
Kipindi cha pili kasi ya mchezo ilipungua huku tukishambuliana kwa zamu lakini hakukuwa na mabadiliko katika ubao wa matangazo.
Kocha Pablo aliwatoa Bocco, Kibu, Pape Sakho, Pascal Wawa, Henock Inonga na kuwaingiza Medie Kagere, Peter Banda, Yusuf Mhilu, Israel Patrick na Kennedy Juma.
Ushindi huu unatufanya kufikisha pointi 49 baada ya kucheza mechi 23 tukiwa nyuma kwa alama nane dhidi ya wanaongoza ligi.