Jitihada haizidi kudra, tunarudi VPL kumalizia kazi

Licha ya ushindi wa mabao 3-0 tuliopata dhidi ya Kaizer Chiefs katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Afrika uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa hatukuweza kutinga Nusu Fainali na kutolewa kwenye mashindano hayo.

Tumetolewa kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya kufungwa 4-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa nchini Afrika Kusini Jumamosi iliyopita.

Tulianza mchezo kwa kasi na kuliandama lango la Kaizer huku tukitengeneza nafasi nyingi lakini hatukuweza kuzitumia ipasavyo.

Nahodha John Bocco alitufungia bao la kwanza dakika ya 23 kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya pasi ya kichwa iliyopigwa na Luis Miquissone.

Kocha Didier Gomes alifanya mabadiliko ya lazima dakika ya 35 baada ya kiungo Taddeo Lwanga na mlinzi Joash Onyango kugongana katika jitihada za kuokoa na kushindwa kuendelea na mchezo.

Bocco alitupatia bao la pili dakika ya 56 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Miquissone kutoka upande wa kushoto.

Clatous Chama alitufungia bao la tatu dakika ya 85 baada ya kupiga chenga walinzi wa Kaizer kabla ya kumchambua mlinda mlango Bruce Bvuma.

Kocha Gomes aliwatoa Mzamiru, Onyango na Taddeo na kuwaingiza Bernard Morrison, Erasto Nyoni na Kennedy Juma.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

  1. timu imecheza vizuri sana pongezi kwa wachezaji,benchi la ufundi na uongozi hakika sisi washabiki tumeridhika na upambanaji wa hali ya juu tunaomba timu isivunjwe ila maboresho yanatakiwa hasa kuongeza kiungo mkabaji, beki wa pembeni na wakati bila kusahau mpachika mabao. kama itawezekana hakikisheni prince dube anatua msimbazi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER