Inonga awaita mashabiki kuweka rekodi kwa Mkapa kesho

Mlinzi wa kati Henock Inonga Baka, amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa kesho wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaopigwa saa 10 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuwapa sapoti wachezaji.

Inonga amesema anaamini mchezo utakuwa mgumu na wachezaji wapo tayari kuhakikisha ushindi unapatikana na kuweka rekodi ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Ameongeza kuwa mchezo wa kesho ni muhimu kwa kila mmoja ndiyo sababu ya kuwaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kuweka rekodi kwa pamoja.

“Mimi nawataka mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho, najua Simba ina mashabiki wengi ni mechi muhimu na tunahitaji kushinda ili kupata nafasi ya kuingia hatua ya makundi hivyo tunahitaji sapoti yao,” amesema Inonga.

Tayari uongozi wa klabu umeainisha maeneo mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam ambayo tiketi zinapatikana kwa ajili ya mchezo huo hivyo mashabiki wetu wanapaswa kukata mapema ili kuepuka usumbufu kesho uwanjani.

Kama tutafanikiwa kushinda mchezo wa kesho tutakuwa tumepata tiketi ya kuingia hatua ya makundi ambapo itakuwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kufika robo fainali.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER