Inonga agawa tuzo yake kwa mashabiki

Mlinzi wa kati Henock Inonga, ameamua kugawa tuzo yake ya mchezaji bora wa mashabiki wa mwezi Aprili (Emirate Aluminium ACP Simba Fans Player of the Month) kwa mashabiki kutokana na sapoti kubwa wanayompa.

Inonga amekabidhiwa tuzo hiyo na wadhamini Emirate Aluminium ACP ambapo pamoja na kuwashukuru wachezaji wenzake lakini pia ameweka wazi anaitoa kwa mashabiki.

“Hili ni jambo kubwa kwangu, inaniongezea morali kuendelea kuipambania timu. Nawashukuru Emirate Aluminium ACP kwa tuzo hii, nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano walionipa lakini naitoa kwa mashabiki,” amesema Inonga.

Kwa upande wake Ofisa Mahusiano wa Emirate Aluminium, Issa Maeda amesema Inonga amekuwa kwenye kiwango bora na kila mtu ameona kutokana na kiwango alichoonyesha.

Aidha, Maeda amesema kwa sasa wameshusha bei za bidhaa zao zote ili kuwafanya Watanzania wanaotaka kujenga kununua katika kipindi ambacho gharama za maisha zimezidi kupanda.

“Inonga amekuwa kwenye kiwango bora mwezi Aprili na kila mmoja ameliona. Tuzo hizi zinatufanya tutangazike kote ndani na nje nchi na tunajivunia kufanya kazi Simba.

“Ingawa Simba imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini kiwango walichoonyesha kila mtu amekubali. Kikubwa naendelea kuwasisitiza Watanzania kuendelea kununua bidhaa zetu,” amesema Maeda.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER