Kikosi chetu leo kinashuka dimbani kucheza mechi ya nusu fainali ya Michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Azam FC utakaopigwa Uwanja wa Majimaji hapa Songea saa tisa alasiri.
Benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki wetu wanaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa wapinzani lakini hata hivyo tuna matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.
Kocha Mkuu, Didier Gomes ameweka wazi kuwa malengo yetu msimu huu yalikuwa kutwaa mataji yote ya ndani hivyo tutapigana kwa kila njia kuhakikisha tunafanikisha.
“Tangu mwanzo wa msimu lengo letu lilikuwa ni kutetea taji hili na tumefika hatua hii kwa hiyo tumejipanga kushinda na kuingia fainali.
“Azam ni timu nzuri na tunakumbuka mchezo wa mwisho tulipokutana nao tuliweza kumiliki mchezo ila tulipoteza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza lakini tumejitahidi kuondoa mapungufu kama hayo ili kupata ushindi leo,” amesema Kocha Gomes.
Kwa upande wake Nahodha, John Bocco amesema wachezaji wote wana ari na kila mmoja atakayepewa nafasi ya kucheza yupo tayari kuipigania timu.
NI MECHI YA KISASI
Tulipokutana katika mchezo wa mwisho ligi kuu mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 7, mwaka huu tulitoka sare ya mabao 2-2 hivyo kila timu itataka kushinda ili kuonekana mbabe na ndiyo kisasi chenyewe.
SAFARI YETU HADI KUFIKIA LEO
HATUA YA 64 BORA
Simba 5-0 Majimaji
HATUA YA 32 BORA
African Lyon 0-3 Simba
HATUA YA 16 BORA
Simba 2-1 Kagera Sugar
HATUA YA ROBO FAINALI
Simba 3-0 Dodoma Jiji
Mshindi wa mchezo wa leo atakutana na Yanga katika mchezo wa fainali utakaopigwa Julai 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
One Response
Ee mwenyezi Mungu tusaidie tuweze kupata pointi tatu kwa mechi hii ya leo