Hongereni Wanasimba tamasha limefana

 

Tamasha letu la Simba Day mwaka 2022 limefana huku tukifikia malengo tuliyokuwa tumejiwekea kwa asilimia 100.

Katuka tamasha hilo, Wanasimba wamejitokeza kwa wingi ambapo hadi saa nane mchana walikuwa tayari wameujaza uwanja mzima wa Benjamin Mkapa ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Kila kitu kilienda sawa kuanzia mpangilio wa matukio, ubunifu uliotumika hali iliyowafanya mashabiki kufurahia kuanzia mwanzo hadi mwisho.

U20 YAFUNGUA TAMASHA

Timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ilikuwa ya kwanza kufungua tamasha letu la Simba Day kwa kucheza mchezo wa kirafiki na Kituo cha Soka cha Rajaa na kutoka sare ya kufungana bao moja.

Vijana hao wa Kocha Mussa Mgosi walionyesha kiwango safi lakini changamoto yao ikawa kutumia nafasi walizotengeneza.

BONGO MOVIE YAICHAKAZA BONGO FLEVA

Mchezo wa pili ambao ulivuta hisia za watu wengi ulikuwa kati ya Bongo Movie dhidi ya Bongo Fleva huku tukishuhudia Bongo Movie wakiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Katika mechi hiyo kilichowafurahisha mashabiki ambao muda mwingi walikuwa wakishangilia ni kutokana na kuwajua mastaa hao ambao wenginwao wamekuwa wakiwaona kupitia runinga.

QUEENS YAICHAKAZA FOUNTAIN

Timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa tatu wa kirafiki.

Mchezo ulikuwa mgumu huku kila timu ikionyesha uwezo wake lakini vijana wa Kocha Sebastian Nkoma walifanikiwa kutumia vizuri nafasi mbili walizopata.

HALAIKI YA WATOTO

Kivutio kingine kilikuwa watoto wa halaiki ambao walionyesha umaridadi mkubwa wa kuchora maumbo mbalimbali ambayo yalinogesha tamasha.

Miongoni mwa maumbo waliyochora ni NGUVU MOJA, ASANTENI WANASIMBA, ASANTE MO DEWJI.

ZUCHU AFUNIKA

Zuchu ametudhihirishia kuwa hatukufanya makosa kumfanya nyota wetu wa burudani kwebye tamasha la mwaka huu.

Alifanikiwa kuwapagawisha mashabiki huku akiamsha shangwe zaidi wakati wa kutua na kamba kutoka juu ya paa la uwanja mpaka chini.

MCHEZO DHIDI YA ST. GEORGE

Mchezo wa kuhitimisha tamasha letu ulikuwa dhidi ya St. George ambapo tulifanikiwa kushinda mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa kwa mabao 2-0.

Tulicheza vizuri na wapinzani wetu walikuwa bora na kutupa wakati mgumu.

Kipindi cha pili tulikuwa bora zaidi, tukiongeza kasi hasa baada ya kuingia viungo washambuliaji Clatous Chama na Nelson Okwa.

Mlinda mlango Beno Kakolanya alikuwa kwenye kiwango bora akipambana vilivyo kuhakikisha anaondoka na ‘clean sheet’ na alifanikiwa.

Kakolanya ameokoa zaidi ya michomo mitano ya hatari ambayo ilikuwa inaelekea wavuni.

TUNDAMAN AJA NA BONGE LA ‘SAPRAIZI’

Mmoja wa wasanii vipenzi vya Wanasimba ni Tundaman ambaye amekuwa akitunga nyimbo mbalimbali za kuisifia timu hatua inayomfanya kupendwa na Wanasimba.

Tundaman alipanda jukwaani akiwa ndani ya jeneza huku Stan Bakora akiingiza kama mchungaji kitu ambacho kilivutia wengi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER