Hizi hapa mechi zilizotupeleka makundi Afrika

Jana tumefahamu tutacheza na mabingwa wa Zambia Power Dynamos katika hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/24.

Mechi ya kwanza itapigwa kati ya Septemba 15-17 nchini Zambia wakati marudiano yatakuwa kati ya Septemba 29-30 jijini Dar es Salaam na mshindi wa jumla atafanikiwa kutinga hatua ya makundi.

Mpaka sasa tiketi yetu ya hatua ya makundi ameishikilia Power Dynamos na kazi iliyombele yetu ni kuhakikisha tunaichukua.

Hizi hapa mechi tatu za kukumbukwa zilizotupeleka hatua ya makundi….

Nkana Red Devil vs Simba (2018)

Mchezo wa kwanza ulipigwa nchini Zambia, Disemba 15, 2018 ambapo tulipoteza kwa mabao 2-1 huku la kwetu likifungwa na nahodha John Bocco kwa mkwaju wa penati dakika ya 73.

Mchezo wa pili ulipigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Disemba 23, 2018 tukaibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mchezo huu unakumbukwa sana kutokana na msako tuliowapiga Nkana huku bao safi la kisigino lililotupa ushindi likifungwa kiufundi na Clatous Chama (89′). Mabao mengine yalifungwa na Jonas Mkude (29′) Medie Kagere (45′)

FC Platinum vs Simba (2020)

Mchezo wa kwanza ulipigwa, Disemba 23, 2020 nchini Zimbabwe na tulipoteza kwa bao moja lililofungwa na Perfect Chikwende ambaye baadae tulimsajili.

Mechi ya marudiano ilipigwa Januari 6, 2021 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa tukaibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Mabao yetu yaliwekwa kambani na Erasto Nyoni kwa mkwaju wa penati (38′), Shomari Kapombe (61′), John Bocco (90′) Clatous Chama (90+5 pen).

C.D Primiero De Agosto vs Simba (2022)

Mchezo wa kwanza ulipigwa nchini Angola, Oktoba 9, 2022 tukaibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Mabao hayo yalifungwa na Clatous Chama (9′), Israel Patrick (63′) na Moses Phiri (75′).

Mchezo wa pili ulipigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Oktoba 16, 2022 tukaibuka na ushindi wa bao lilifungwa na Moses Phiri.

Chama ni mwamba wa mechi hizi….

Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama mara zote ameibuka shujaa kwenye mechi za kufuzu kuingia hatua za makundi.

Ukiachilia mbali kuonyesha kiwango safi lakini amehusika na mabao katika kila mchezo huku mwenyewe akitupia matatu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER