Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema katika mchezo wa kesho wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli kutoka Libya tutacheza kwa umakini mkubwa.
Kocha Fadlu amesema tutacheza kwa umakini mkubwa hasa katika safu ya ulinzi kwani hatupaswi kuruhusu bao huku pia tukitakiwa kuhakikisha tunapata mabao zaidi.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa itakuwa mechi ngumu lakini tutakuwa na faida kwakuwa tupo nyumbani na mashabiki wetu watakuwa nyuma yetu.
Akizungumzia hali ya kikosi kocha Fadlu amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri isispokuwa Mzamiru Yassin ambaye alipata maumivu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ingawa anaendelea vizuri.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, itakuwa mechi ngumu kwakuwa inahusisha timu mbili kubwa ambazo sio tu zinawaza kuingia hatua ya makundi bali kuchukua ubingwa wenyewe,” amesema Kocha Fadlu.
Nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wa wachezaji wapo tayari kuhakikisha wanapambana ili kuiwezesha timu kuingia hatua ya makundi.
“Hali kama hii imewahi kututokea mara nyingi huko nyuma na hatuna presha tunajua Wanasimba wanahitaji furaha nasi tupo hapa kuhakikisha hilo linafanikiwa,” amesema Zimbwe Jr.