Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2022/23 itapangwa Jumatano, Aprili 5 jijini Cairo, Misri saa tatu usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Droo itafanyika mubashara kupitia mitandao ya kijamii ya CAF pamoja na TV washirika wa Shirikisho hilo.
Mechi za mwisho za hatua ya makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika zimekamilika mwishoni mwa wiki hii na tayari zilizomaliza kwenye nafasi mbili za juu kwenye kila kundi zimejulikana.
Hizi hapa timu nane zilizofanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali.
CR Belouizdad (Algeria), Esperance Tunis (Tunisia), JS Kabylie (Algeria), Mamelodi Sundowns (South Africa), Raja CA (Morocco), Simba SC (Tanzania), Wydad AC (Morocco) na Al Ahly (Egypt).