Bwalya aeleza furaha ya kutupia bao lake la kwanza Mabingwa Afrika

Kiungo mshambuliaji Rally Bwalya ameeleza furaha yake ya kufunga bao lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa ndani ya kikosi chetu ambalo limechangia kutupeleka robo fainali ya michuano hii.

Bwalya alifunga bao hilo akitokea benchi dakika ya 66 kwa shuti kali la mguu wa kushoto nje kidogo ya 18 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Clatous Chama kwenye mchezo wa jana dhidi ya AS Vita.

Bwalya raia wa Zambia ameongeza kuwa ni furaha kwake kufunga kwenye mechi muhimu ambayo imeamua hatima ya kutinga robo fainali.

“Ni furaha kubwa kufunga bao kwenye mechi muhimu ya Klabu Bingwa Afrika, hili ni bao langu la kwanza katika michuano hii na imekuwa vizuri pia kwa kuwa ni mechi ya maamuzi ambayo imetupeleka robo fainali,” amesema Bwalya.

Baada ya kufanikiwa kutinga Robo Fainali, Bwalya amesema wao kama wachezaji wanajiandaa kuhakikisha tunafanya vema ili kuingia nusu na hatimaye fainali yenyewe.

“Kwa sasa malengo yetu kama wachezaji ni kuhakikisha tunaingia nusu fainali kisha fainali. Tumeona inawezekana na tutajitahidi kulifanikisha hilo,” amesema Bwalya.

Kiungo huyo fundi anayetumia mguu wa kushoto amewashukuru mashabiki wetu kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika hali zote iwe mbaya au nzuri kwani wakati mwingine mpira una matokeo ambayo hayafurahishi na bado wapo pamoja na timu.

SHARE :
Facebook
Twitter

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER