Bocco, Mkude fiti kuivaa Prisons kesho

Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola amesema Nahodha John Bocco na kiungo Jonas Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliosafiri kuelekea jijini Mbeya tayari kwa mchezo wa kesho wa ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons.

Matola ameyasema hayo akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) muda mfupi kabla ya kupaa kuelekea Mbeya huku akisema wachezaji wengine wote pia wapo kwenye hali nzuri.

Nahodha Bocco yeye alishaanza kuonekana akiwa benchi katika mechi mbili zilizopita lakini Mkude amekosekana muda mrefu kutokana na kuwa na majeruhi lakini sasa yupo kamili kuipigania timu.

Matola amesema tumeamua kuondoka siku moja kabla ya mchezo kwa kuwa tunajua Uwanja wa Sokoine leo una mechi nyingine kwa hiyo hata kama tungewahi tusingepata nafasi ya kufanya mazoezi hivyo tulifanya Mo Arena asubuhi ndio tukaanza safari.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu, mara zote tukikutana na Prisons mechi inakuwa ngumu hasa wakiwa Sokoine lakini safari hii itakuwa ngumu zaidi sababu hawapo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo hivyo watataka kupata pointi tatu kutoka kwetu lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Matola.

Matola amesema katika mchezo wa kesho tutawakosa mlinda mlango Aishi Manula (ana matatizo ya kifamilia), Pape Sakho (ameumia bega) na Sadio Kanoute (ameenda nchini kwao kufuatilia passport yake ambayo imeisha muda wake).

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER