Bocco akabidhiwa ‘mpunga’ wake na Aluminium Profile

Nahodha John Bocco amekabidhiwa kitita cha Sh 2,500,000 na Kampuni ya Emirate Aluminium Profile baada ya kuibuka mchezaji bora katika mchezo wa marudiano Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs.

Katika mchezo huo uliopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 Bocco alitupia mawili huku akionyesha kiwango bora.

Emirate Aluminum iliahidi ya kiasi hicho kwa mchezaji bora wa mechi zote mbili ya ugenini na nyumbani za robo fainali ili kuongeza hamasa kwa wachezaji.

Baada ya kukabidhiwa kiasi hicho Bocco amewashukuru wachezaji wenzake, benchi la ufundi na mashabiki kwa ushirikiano aliopata maana bila wao asingeweza kufikia lengo hilo.

Bocco pia ameishukuru Emirate kwa sababu imeongeza hamasa kwa wachezaji na kuendeleza ari ya kuipambania timu na mafanikio yake yanazidi kuonekana.

“Nawashukuru wachezaji wenzangu, benchi la ufundi na mashabiki kwa ushirikiano huu, pia nawashukuru Emirate kwa kuongeza hamasa na ni jambo jema na mafanikio yake yanaonekana,” amesema Bocco.

Kwa upande wake Afisa Mahusiano wa Emirate Aluminum, Issa Maeda amesema lengo la kutoa kiasi hicho cha fedha ni kutaka kuiona Simba inafanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuingia Nusu Fainali ingawa kwa bahati mbaya haikufanikiwa.

“Tuliahidi kutoa Sh 2,500,000 kwa mchezaji bora wa kila mechi kwenye hatua ya Robo Fainali. Mchezo wa kwanza kule Afrika Kusini hatukutoa sababu kila mtu aliona kilichotokea.

“Ila mechi ya Jumamosi kila mtu alishuhudia jinsi wachezaji walivyofanya na takwimu zinambeba zaidi Bocco na tumemkabidhi zawadi yake leo amesema Maeda.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER