Baada ya kumaliza mechi tatu mfululizo za Kanda ya Ziwa nakupata alama zote tisa, kikosi chetu leo kitashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Dodoma Jiji.
Kuelekea mchezo wa leo kocha msaidizi, Seleman Matola amesema kikosi kipo kwenye hali nzuri wachezaji wamefanya mazoezi ya mwisho na jambo jema ni kwamba wako vizuri.
Matola ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu na tunawaheshimu Dodoma lakini tunahitaji kutimiza malengo ya kutetea ubingwa hivyo tunapaswa kushinda kila mechi.
“Dodoma Jiji ni timu nzuri lakini pamoja na ugumu na ubora wao lazima tupate alama tatu. Kila timu ambayo tunakutana nayo tunaenda kucheza kama fainali, tumeshasema nia yetu ni kutetea ubingwa,” amesema Matola.
TAARIFA YA KIKOSI
Nyota wawili kiungo mshambuliaji Luis Miquissone na mlinzi wa kati Pascal Wawa wamerejea kikosini baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Gwambina FC kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Kiungo Taddeo Lwanga ndiye pekee atakayekosekana kwenye mchezo wa leo kutokana na kusafiri kwenda Uganda baada ya kufiwa na dada yake wiki iliyopita.
MATOKEO YA MECHI ILIYOPITA TULIVYOKUTANA
Katika mchezo wa mzunguko kwa kwanza uliochezwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Februari 4, mwaka huu tuliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Mabao yetu yalifungwa na Medie Kagere na Bernard Morrison huku la kwao likifungwa na Cleophas Mkandala.