Kiungo mshambuliaji, Said Ntibazonkiza amefurahia kumaliza msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2022/23 kwa kuibuka kinara wa ufungaji kwa kutupia nyavuni mabao 17.
Ntibazonkiza amewashukuru wachezaji wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliompa hadi kufanikiwa kumaliza kinara wa ufungaji.
“Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa, sio kwa uwezo wetu bali ni majaaliwa yake. Pili nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano mkubwa walionipa mpaka kufika leo.
“Nina furaha lakini tulitamani kupata mataji ingawa haikuwa hivyo, tunajipanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, naamini viongozi wameona timu ilivyo na watafanya maboresho kuelekea msimu ujao,” amesema Ntibazonkiza.
Ntibazonkiza ambaye tumemsajili kutoka Geita Gold katika dirisha dogo la usajili mwezi Novemba alikuwa amefunga mabao sita hivyo mengine 11 ametupia akiwa ndani ya kikosi chetu.
Ntibazonkiza amelingana na mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele ambaye nae amefunga mabao 17.