Alichosema Kocha Matola kuelekea mchezo na KMC

Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola, amesema morali ya wachezaji ipo juu kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya KMC licha ya kuwa bingwa wa ligi amepatikana.

Matola amesema wachezaji wetu ni wa kimataifa hivyo wanajua umuhimu wa kutafuta pointi tatu katika kila mchezo mpaka ligi imalizike.

Matola amesema KMC ni timu nzuri na inatupa ushindani kila tukikutana lakini tutahakikisha tunatumia mapungufu yao na kujikinga na ubora wao ili tupate pointi zote tatu kesho.

“Baada ya mchezo na Mbeya City tumepata siku mbili za mazoezi, wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mchezo. Tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kuwakabili.

“Simba ni timu kubwa inahitaji kushinda kila mchezo hata kama wa kirafiki na wachezaji wanalijua hilo, nilisema mwanzoni kuwa tunahitaji kumaliza ligi kwa heshima,” amesema Matola.

Kuhusu hali ya kiungo mshambuliaji Clatous Chama amesema ameanza mazoezi na wenzake lakini hayuko timamu asilimia 100 hivyo hatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho.

“Chama ameanza mazoezi pamoja na wenzake lakini hayupo fiti kwa hiyo hatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho badala yake ataanza kuonekana mechi zijazo,” amesema Matola.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER