Kocha Mkuu, Charles Lukula amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wetu wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Determine Girls kutoka Libya utakaopigwa kesho saa 11 jioni nchini Morocco.
Lukula amesema anaamini kikosi chetu kitafanya vizuri kwenye mchezo huo na wameyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza tuliyopoteza.
Katika mazoezi ya siku mbili tuliyofanya baada ya mchezo wa kwanza Lukula na wasaidizi wake wameongeza msisitizo kwenye kutumia nafasi tunazotengeneza na kuzuia kwa pamoja.
“Hata ukiangalia kwenye mchezo wa kwanza tulicheza vizuri na tulipata nafasi lakini hatukizitumia, na lile bao tuliloruhusu lilitokana na timu kuchelewa kujipanga kwahiyo tumeyaona mapungufu na tumeyafanyia kazi,” amesema Lukula.
Kwa upande wake mshambuliaji Olaiya Barakat amesema morali yao ipo juu na matokeo ya mchezo wa kwanza hayaja wachanganya na wapo tayari kupambana kupata pointi tatu muhimu.
“Walimu wetu wametuelekeza tunachotakiwa kukifanya nasi tupo tayari kwenda kukitekeleza uwanjani, tuna matumaini ya kuhakikisha tunashinda,” amesema Olaiya.