Alichosema Kocha Fadlu kuelekea mchezo wa dhidi ya Coastal

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Coastal utakaopigwa katika Uwanja wa KMC Complex saa 10:15 jioni utakuwa mgumu.

Fadlu amesema amewatazama Coastal katika mechi zao walizocheza siku za karibuni wamekuwa wakibadilika kiuchezaji na kushambulia kwa kasi kitu ambacho tutahakikisha tunachukua tahadhari.

Akizungumzia hali ya kikosi kocha Fadlu amesema anatarajia kuwepo kwa mabadiliko kadhaa ya wachezaji kutokana na ratiba kuwa ngumu ambapo tunacheza mechi tatu ndani ya wiki moja.

“Siwezi kusema nitampanga mchezaji gani au nani hatakuwepo kesho kwakuwa ratiba ni ngumu. Tunatengeneza uwiano wa wachezaji kwakuwa kuelekea Disemba ratiba itakuwa ngumu zaidi.

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo, hauwezi kuwa bingwa kwa kushinda mechi nne, tunatakiwa kuendelea kukusanya pointi na kuhakikisha tunaweza pia kuzuia vizuri,” amesema Kocha Fadlu.

Kwa upande wake nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo watayopewa ili kuisaidia timu kupata ushindi.

“Sisi wachezaji tupo tayari, tunaiheshimu Coastal kutokana na ubora wao ila lengo letu ni kuhakikisha tunashinda tukiwa nyumbani na kuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Zimbwe Jr.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER