Uongozi wa klabu umefikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu na mlinda mlango namba moja, Aishi Manula utakaomuweka Msimbazi hadi mwaka 2025.
Aishi amefanikiwa kutunza kiwango chake kwa muda mrefu ambapo amechukua tuzo ya mlinda mlango bora wa Ligi kwa misimu minne mfululizo.
Aishi ni mmoja ya wachezaji wazawa ndani ya kikosi chetu ambao wamejihakikishia nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kwa muda mrefu.
Kuelekea msimu mpya wa ligi 2022/23 tunaendelea kuimarisha kikosi ikiwemo kuwaongezea mikataba wachezaji ambao tunaamini bado ni msaada mkubwa kwetu.
Ushindani wa kuinasa saini ya Manula ulikua mkubwa baada ya kuwa anahitajika na vilabu kadhaa vya nje ya nchi na hapa nyumbani
Kwa kutambua umuhimu na ubora wa mlinda mlango huyo klabu ikaamua kumuongezea mkataba wa muda mrefu zaidi
Katika kipindi cha miaka mitano Manula ameiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania mara nne mfululizo, Ubingwa wa Kombe la Shirikisho mara 2 pamoja na kucheza robo fainali tatu za michuano ya Afrika
Kwa sasa Aish Manula yupo kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania na atajiunga na wenzie mwishoni mwa mwezi huuu