‘Ahsanteni kwa kutulindia nafasi yetu, hatushuki ng’ooo hadi ubingwa’

Bao pekee lililofungwa na Nahodha Msaidizi, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Junior’ katika mchezo dhidi ya Gwambina FC, limetosha kutupandisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom tukifikisha alama 58.

Zimbwe alifunga bao hilo kwa shuti kali la nje 18 lililomshinda mlinda wa Gwambina, Mohammed Makaka na kugonga mwamba wa juu kabla ya kuingia wavuni moja kwa moja.

Katika mchezo wa leo tulicheza zaidi mipira mirefu ya juu kitu ambacho si kawaida yetu kutokana na uwanja kutokuwa rafiki kuruhusu pasi fupi fupi (pira biriani).

Dakika ya 74 mlinzi Joash Onyango alifunga bao la kichwa akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Clatous Chama lakini mwamuzi msaidizi namba moja alilikataa kwa kusema mpira ulitoka kabla kufungwa.

Kocha Didier Gomez aliwapumzisha Bernard Morrison, John Bocco na Medie Kagere kuwaingiza Hassan Dilunga, Chris Mugalu pamoja na Jonas Mkude.

Ushindi wa leo unatufanya kukamilisha malengo yetu ya kuondoka na alama zote tisa za mechi tatu za Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui FC, Kagera Sugar na leo Gwambina.

Hii ni mara ya kwanza msimu huu na kwetu kukalia usukani wa ligi kuu ambapo tunaongoza kwa tofauti ya alama moja huku tukiwa na michezo miwili mkononi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER