Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema lengo la kuileta mechi yetu ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC ni kuwathamini mashabiki wetu wa Mkoa wa Mwanza ambao hawapati muda mwingi wa kuiona timu yao.
Ahmed ameyasema hayo wakati wa hamasa ya kuzunguka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Mwanza ili kuwakumbusha mashabiki kujitokeza kwa wingi kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba.
Ahmed mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa sehemu ambazo tuna mashabiki wengi kwahiyo tumeipeleka mechi hiyo kubwa tukiwa tunajua tutapata msaada mkubwa kutoka kwa mashabiki.
“Tumeleta mechi Mwanza kwa kutambua umuhimu na thamani yenu. Tunajua nguvu yenu hakuna linaloshindikana.
“Tumejiandaa vizuri kupata matokeo lakini haitakuwa rahisi tukiwa peke yetu, lazima Wanasimba tushikamane, tuungane tukapate matokeo kwa pamoja,” amesema Ahmed.
Ahmed ameendelea kwa kusema kuwa “Wanasimba wa Mwanza mna bahati sana ya kwenda kuiona Simba ikiwa ya moto. Wakati wengine wameshuka, Simba tumepanda. Wakati wao wanaumaliza mwendo, pumzi ya Mnyama imejaa. Simba imekuja ikiwa ya moto kwelikweli, Simba hii haina presha.”