Ahmed: Tumedhamiria kuwafunga Yanga Jumapili

Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amesema dhamira yetu nikuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wa Derby ya Kariakoo dhidi ya Yanga utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5 saa 11 jioni.

Ahmed amesema viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wapo tayari kuhakikisha tunapambana na kupata ushindi na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo.

Ahmed ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu hasa ukiangalia ubora wa wapinzani wetu ingawa tumejipanga kuwapa furaha mashabiki wetu.

“Jumapili tunashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo muhimu ambapo ushindi wake unashangiliwa mpaka mechi nyingine itakapofika.

“Huu ni mchezo mkubwa ambao furaha na huzuni yake hudumu kwa muda mrefu kwahiyo tunajipanga kuhakikisha furaha inakuwa upande wetu,” amesema Ahmed.

Ahmed amewaomba mashabiki wa timu hizo kuwa wastarabu na kutaniana kwa heshima ili kusitokee vurugu ili aliyejiandaa vizuri apate ushindi halali uwanjani.

“Tunawasihi mashabiki wetu pamoja na wale wa Yanga kuhakikisha wanataniana kistaarabu na kuhakikisha hawavuki mipaka yao katika utani.

“Tunalaani kitendo cha mashabiki waliopigana katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Ihefu FC, hatujui sababu ya chanzo cha tukio lakini pamoja na yote hatujapendezwa na kilichotokea,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER