Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewaongoza wanachama, wapenzi na mashabiki wetu kuchangia damu ikiwa ni sehemu ya shughuli ya kijamii kuelekea kilele cha Simba Day Agosti 8, mwaka huu.
Zoezi hili la uchangiaji damu ni la nchi nzima lakini jijini Dar es Salaam tumekuwa na vituo viwili ambavyo ni Makao Makuu ya Klabu Msimbazi Karikakoo na Mbagala Zakhiem.
Baada ya kuchangia damu Ahmed amesema uongozi umeona ni jambo jema linalompendeza hata Mungu kuokoa maisha ya watu ndiyo maana limekuwa zoezi la nchi nzima.
“Hakuna sehemu yoyote kuna kiwanda cha damu duniani bali inapatikana kwa kuchangiana ndiyo maana uongozi wa klabu tumeamua kuifanya nchi nzima ikiwa ni sehemu ya wiki ya Simba.
“Ili kuonyesha ukubwa na uzito wa jambo hili mimi mwenyewe nimechangia tayari ili kuokoa maisha ya Wanasimba wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla,” amesema Ahmed.
Katika kuendelea kufanya shughuli za kijamii jana kwa kushirikiana na Mo Dewji Foundation tulitembelea kituo cha kulelea Wazee cha Nungu kilichopo Kigamboni na kutoa misaada mbalimbali kama unga, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni ya unga na sabuni za miche.