Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu, Ahmed Ally amewaambia wapenzi na wanachama wa Chanika Msumbiji kuwa tumekuja huku kutokana na umuhimu wa mchezo wetu wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya.
Ahmed amesema Wanasimba wengi wanaokaa Chanika hawana utaratibu wa kwenda uwanjani kwakuwa wanaona wanaishi mbali hivyo zoezi la kuisapoti timu ni la Wanasimba wengine.
Ahmed ameongeza kuwa mchezo wa Jumamosi ni muhimu sana kwetu ndio maana tumekuja hadi Chanika kuwaomba Wanasimba tujitokeze kwa wingi kwa Mkapa ili kuisapoti timu.
“Mchezo wa Jumamosi dhidi ya Horoya ni muhimu na mgumu, tunajua kama tutajitokeza mashabiki 60,000 kwa Mkapa Horoya hata wawe bora vipi hawatoki.”
“Tumekuja hadi huku lengo ni moja kuwaomba Wanachanika na viunga vyake mje kwa wingi uwanjani Jumamosi ili tuisapoti timu itinge robo fainali.
“Itakuwa ni fedheha kubwa kama tutashindwa kuifunga Horoya tukaishia hatua hii ya makundi, hii ni ya kwetu wote Wanasimba na ndio maana tupo hapa Chanika leo sisi wote tuliopo hapa tukutane kwa Mkapa Jumamosi,” amesema Ahmed.